Welcome to TANZANET - General Information  

The TANZANET Kandoro Prize

 
Tanzania pictures

Tanzania


TANZANET-KANDORO PRIZE
[ main page | Guidelines | Biographical Note | Award 2002 | Award 2003 ]

Tuzo ya Kandoro mwaka 2003 ametunukiwa mshairi Amiri Sudi Andanenga "Sauti ya Kiza"

Jopo la TANZANET la Tuzo ya Kandoro linayo furaha kutangaza kuwa tuzo ya Mwaka 2003 ametunukiwa mshairi Amiri Sudi Andanenga "Sauti ya Kiza" wa Kinondoni Shamba, Dar-es-Salaam Tanzania. Mshairi Amir S. Andanenga ametunukiwa tuzo la Mwaka 2003 kwa kuzingatia mchango wake katika ushairi na lugha ya Kiswahili.

Mshairi Amiri S. Andanenga alizaliwa Tarehe 02-Oktoba-1936 katika kitongoji cha Nanyati mjini Kilwa. Tangu ujana wake Sauti ya Kiza ameshiriki katika malumbano ya tenzi na Ushairi na aliwahi kutunukiwa zawadi mbalimbali zikiwepo zile zilizotolewa na BBC, Chama cha Usanifu wa Ushairi na Kiswahili, na Tuzo ya Zeze.

Umahiri wa Andanenga unajidhihirisha kutoka katika vitabu vyake ’Diwani ya Ustadhi Andanenga,’ na kile cha ’Bahari ya Elimu ya Ushairi’ vitabu hivi viwili vimedurusu masuala mbalimbali, ikiwepo elimu bora ya ushairi na kiswahili.

Mbali ya uandishi unatoka katika utamaduni wa tenzi za Kiswahili, mpangalio wa beti za mistari minne-minne, Andanenga alikuwa ni miongoni mwa washairi wa kwanza kupambana kimalumbano na ujio wa nyanja mpya za ushairi inayojulikana kama mashairi kimapokezi.

Kwa kuzingatia mchango wake kwa ujumla, wanajopo wa Tuzo ya Kandoro kwa niaba ya TANZANET, wanamzawadia tunu ya mwaka 2003 Mshairi Amiri Sudi Andanenga (Sauti ya Kiza).

Picha za tuzo la mwaka 2003

Dr. Aziz P. Mlima
Chairperson-Kandoro Prize Committee, 2003


The TANZANET Kandoro-Prize 2003 is awarded to poet Amiri Sudi Andanenga "Sauti ya Kiza"

The TANZANET Kandoro-Prize 2003 is awarded to poet Amiri Sudi Andanenga of Kinondoni Shamba Dar Es Salaam, Tanzania. The prize has been awarded in recognition of the poet´s mastery of Kiswahili verse and, contribution to the language.

Amiri Sudi Andanenga (Sauti ya Kiza) was born 1936 in Nanyati, Kilwa. He has spent most of his adult life in Dar Es Salaam. He has produced an extensive body of work in newspapers and for the radio. His epic work ’Diwani ya Ustadhi Andanenga’, and ’Bahari ya Elimu ya Ushairi’ Andanenga continues the grand lineage of 20th Century Kiswahili poetry narration with a brilliant interweave of panoramic spiritual information with political-economic chronicle of Tanzanian society.

His uncompromising distaste for rhetoric and his almost prosaic frugality in the use of metaphors and reintroduction of epigrammatic and dramatic modes, updated Kiswahili poetry for the post-Shaaban Roberts´ verse for the 21th Century. These attributes, introduced by renowned Kiswahili poets Sheikh Amri Abeid and Saadani A. Kandoro found their true bearer in Andanenga. And like all those bearers of a truly human truly transforming art, his poetry is deeply impure, deeply defiant and deeply seeking and absolutely clear that the verse must be truth to the human condition and beauty.

Kandoro-Prize Committee, on behalf of the TANZANET Community, awards 2003 Kandoro Prize to Amiri Sudi Andanenga (Sauti ya Kiza).

2003 Presentation pictures

Dr. Aziz P. Mlima
Chairperson-Kandoro Prize Committee, 2003

Members of the TANZANET-Kandoro Prize Committee (2003)

Dr. Aziz P. Mlima (Chairperson II (2002-3)
Mr. Yusuf Kalala (Chairperson I (2001)
Mr. Thabit Tambwe (Secretary)
Dr. Balla Maselle (Member)
Ms. Getrude N. Malai (Member)
Ms. Saada Al-Ghafry (Member)
Dr. Hassan O. Ali (Member)
Mr. Henry Mgaya (Member)
Mr. Richard Madete (Member)

Mailing list:  kandoro-prize@tanzanet.org


Baadhi ya mashairi ya "Sauti ya Kiza"

"KUTENDANA"

Niufungue mfundo, niloutunga sana,
Haufanguki kwa nyundo, ya utunzi wenye kina,
Kutaeda ni kutendana, tenda na mimi nitende,

Nipa na mimi nikupe, kupana ni kupeana,
Leo nasema kweupe, si usiku ni mchana,
Ni kwa vyangu unenepe, hutaki kugawizana,
Nyege ni kunyegezana, nyegeza nikunyegeze,

Nyegeza nikunyegeze, nyege ni kunyegazana,
Wataka nikunoneze, hutaki kunonezana,
Nikisema nipuuze, vipi mwanzangu wanuna!
Gawa ni kugawiana, gawa na mimi nigawe

 

HUKU NA KULE

Peni yangu Andanenga, uwino unapotona,
Mantiki huzilenga, na balagha na bayana,
Hufaidika malenga, huvurugika akina,
Nyege ni kunyegezana, msemo wa Kiswahili.

Msemo wa Kiswahili, nyege ni kunyegezana,
Maana yaki kamili, “wema ni kutendeana’,
Wasiojua fasili, hunamba nimetukana,
Nyege ni kunyegezana, msemo wa Kiswahili.

Ni msemo maarufu, ambao shaka hauna,
Kwenye kamusi sanifu, funueni mtaona,
Niwezeje kukashifu, nami mwana muungwana!
Nyege ni kunyegezana, msemo wa Kiswahili.

Ninataja ukurasa, wazi hapa naunena,
Soma mbili moja tisa, soma bila ya fitina,
Msemo siyo wa sasa, si juzi licha wa jana,
Nyege ni kunyegezana, msemo wa Kiswahili.

Ushairi kubwa fani, mithili yake haina,
Kujua zake bayani, yataka kikubwa kina
Muoneni mwafulani, hata kuku wamguna,
Nyege ni kunyegezana, msemo wa Kiswahili.

Ulipotamkwa mlo, kaja akitunatuna,
Akakabwa koromelo, akabaki kugunaguna,
Kabakia lolololo, uzamani umechina,
Nyege ni kunyegezana, msemo wa Kiswahili.

Alhaji Jitukali, pokea pongezi tena,
Kikubwa chako kilili, hapandi yule mtwana,
Atuache tule wali, yeye ugali wa dona,
Nyege ni kunyegezana, msemo wa Kiswahili.

Kaditama wa Busara, na Mbwezi heko kijana,
Pongezi ndugu Kagera, Yobu has ante sana,
Ndimi Mshairi Bora, kipofu ninaeona,
Nyege ni kunyegezana, msemo wa Kiswahili.
(Mshairi Bora)

Amiri A. S. Andanenga (Sauti ya Kiza)
SLP 4775,
Kinondoni Shamba
Dar es Salaam. (*GT)

MOLINA TUPE NGUVUZO

Yaillahi ya-manani, nguvuzo tupe nguvuzo,
Nguvuzo na ihisani, ihisani za mjazo,
Mjazo ni miilini, afya njema tuwe nazo,
Nazo zitupe uwezo, kufika Maabadani.

Maabadani daima, ndiyo yako maagizo
Maagizo yenye wema, wema kwa zemazo,
Zemazo za mapendezo, zitupeleke jannani.

Jannani ndipo mahali, pazuri penye liwazo,
Liwazo la ufadhili, ufadhili wa Jazazo,
Jazazo ziwe kabuli, kwetu sisi Ziumbezo,
Ziumbezo kwa bembezo, tupe mema Ya-Dayani.

Ya-dayani hapa mwish, twaomba masikilizo,
Masikilizo kwa kesho, tuepushe maunguzo,
Maunguzo mapotosha, yawe mbali kwa sogezo
Sogezo na tumezo, tuwe pamoja vitini.

(Mshairi Bora)
Amiri A. S Andanenga (Sauti ya Kiza)
SLP, 4775,  Kinondoni Shamba,
Dar es Salaam.
(Mwananchi, Oktoba 10 ­ 13, 1994) (*GT)

 

SIUMWI MARA YA PILI

1. Sikhofii kutukanwa, nakhofia kutukana,
Vitabuni imenenwa, watu hupata laana,
Madhambi mengi huvunwa, kwa ringo na kujiona,
Siwezi kuramba tena, sumu nalokoswa nayo.

2. Simu nalokoswa nayo, nendeje kuramba tena?
Nifishwapo nayo hiyo, vipi nitaonekana!
Kwa hiyo siku ambayo, wazishi wamekutana?
Kwa hiyo sirambi tena, sumu nalokoswa nayo.

3. Miba nalotonwa mwando, ngozi yangu ikachana,
Ikanitia uvundo, hatibiwa n´kapona,
Siiwekei upendo, mshawasha nayo sina,
Mimi siyendei tena, sumu nalokoswa nayo.

4. Shimo alongiya nyoka, dhahiri siyo kwa dhana,
Yuangiya na kutoka, mwenzangu kagongwa jana,
Katu sitajipeleka, kwa nguvu tutagombana,
Kamwe sitaramba tena, sumu nalokoswa nayo.

5. Tendo lile la awali, tunguze hazitapona,
Ungeomba tafadhali, chombezo kila aina,
Ninaswe mara ya pili, hola! Sitapatikana,
Elewa sirambi tena, sumu nalokoswa nayo.

"Kilimo"

6. Hata shamba kwa kilimo, nitalima kwa namna,
Shamba lisilo na chumo, kulima sitang´ang´ana,
Nitaridhia kihamo, ndaa isijenitona,
Ndomana sirambi tena, sumu nalokoswayo.

7. Nifugeje kwa shauku, ng´ombe wasiyozaana!
Bora nitafuga kuku, nichinje na kutafuna,
Katu sifugi chiriku, kidege nyama hakina,
Nyimboze ni kutukana, ndo sumu ya ndege huyo.

8. Kuishi naye mwerevu, yataka busra pana,
Bali mtu mpumbavu, jibwakoko alingana,
Litupie nyama mbovu, hula kama ilonona,
Tama hamu sina, sumu nalokoswa - nayo

Amiri A.S. Andanenga (Sauti ya Kiza)
Kinondoni-Shamba
Dar es Salaam, Tanzania. (*HAU)

EWE NYONDA WANGU

Nyonda pokea salamu,
Hali yangu mahamumu,
Wewe kutopandwa hamu,
Ya kuja kunisalimu,
Nyonda nyuma angalia,
Uwezo andama njia.

Hali yangu ya mashaka,
Imesha pita miaka,
Nyonda unayo hakika
Nyonda kwa kutonifika,
Kwa hili nalalamika,
Nyonda nyuma angalia,
Upate andama njia.

Nyonda ingerudi jana,
Hiyo nasi kukutana,
Mengi kwako ningenena,
Jana kutokuja tena,
Kwa hili nalia sana,
Nyonda nyuma angalia,
Upate andama njia.

Nyonda nakuita nyonda,
Pendo ulilolipanda,
Moyoni limesha tanda,
Kwa kutochuma matanda,
Kwa hili mimi nakonda,
Nyonda nyuma angalia,
Upate andama njia.

Nyonda utapo jaribu,
Hata kwa dhiki na tabu,
Njoo nyonda mahabubu,
Uone yanonisibu,
Kwa hili utanitibu,
Nyonda nyuma angalia,
Upate andama njia.

Mimi ni kama tumbusi,
Magumu hayanighasi,
Mvumilivu kiasi,
Kingi sina wasiwasi,
Kwa hili nasema basi,
Nyonda nyuma angalia,
Upate andama njia.

(Sauti ya Kiza)
Amiri A. S. Andanenga
August 1981 (*GT)

SERA YA UTAMADUNI (Uzinduzi)

Kwa hadhi na taadhima, nasimama hadharani,
Akina baba na mama, naomba nisikizeni,
Kwenu nitakayosema, kwa kina zingatieni,
Huwa ni Taifa duni, liso na Utamaduni.

Iwapo halitakufa, huwa halina thamani,
Litaisha kwa kashifa, kwa kuiga ya kigeni,
Na hiyo ndiyo maafa, tuyaepuke jamani,
Huwa ni Taifa duni, liso na Utamaduni.

Baada ya kujadili, kwa ndani utafitini,
Tukagundua ukweli, ambao ni wa yakini,
Ndipo kongomano hili, hapa likawaiteni,
Huwa Taifa duni, liso na Utamaduni.

Leo ndio uzinduzi, "Sera ya Utamaduni",
Ili kuiweka wazi, ieleweke Nchini,
Pia ifanyiwe kazi, isibaki vitabuni,
Huwa ni Taifa duni, liso na Utamaduni.

Kama tukiulizana, "Utamaduni ni nini?",
Majibu yatagongana, kutoka mwetu vichwani,
Mbali hayataachana, kwenye yake tathmini,
Huwa ni Taifa duni, liso na Utamaduni.

Utamaduni matendo, hupokewa Taifani,
Na kisha yake mitindo, huenea majimboni,
Yalo na mwema mwenendo, hupokewa Taifani,
Huwa ni Taifa duni, liso na Utamaduni.

Upo ule wa maisha, wa viumbe duniani,
Mfano wa kunyonyesha, kwa wote hatuachani,
Ujumbe kuufikisha, kwa lugha hatulingani,
Huwa ni Taifa duni, liso na Utamaduni.

Tatizo huanza hapa, shina kwenda kileleni,
Ikiwa mtaitupa, lugha yetu jalalani,
Wote mtatapatapa, sawa wafao majini,
Huwa ni Taifa duni, liso na Utamaduni.

Sisi kwa hali na mali, vibwebwe tujifungeni,
Hata iwe bei ghali, tuikabili medani,
Tutetee Kiswahili, kiwe mbele maishani,
Huwa ni Taifa duni, liso na Utamaduni.

Rangi mtu hujulisha, atokako kwa kudhani,
Pengine hukupotosha, sivyo ulivyobaini,
Lugha inathibitisha, utaifa kwa bayani,
Huwa ni Taifa duni, liso na Utamaduni.

Lugha sitetei tuu, sababuye ishikeni,
Lugha ndiyo zana kuu, kwa yote ulimwenguni,
Lugha ipandishwe juu, ufuzu Utamaduni,
Huwa ni Taifa duni, liso na Utamaduni.

Kiswahili himahima, kifundishie shuleni,
Kipate yake heshima, kifundishie vyuoni,
Nguo tunazoazima, hazihifadhi mwilini,
Huwa ni Taifa duni, liso na Utamaduni.

Lugha nyingine masomo, zitieni vipindini,
Na Kiswahili kiwemo, mbinu zake kazieni,
huo ndiwo msimamo, wa kututia "utuni",
Huwa ni Taifa duni, liso na Utamaduni.

Kwamba hakitoshelezi, kamwe sikubaliani,
Lugha gani zako njozi, waota usingizini?
Maneno ya uchafuzi, tuyatupie mbalini,
Huwa ni Taifa duni, liso na Utamaduni.

Yamepitwa na wakati, "eti" yote ya zamani,
Ya sasa ni madhubuti, yote tusiyaamini,
Kubwia mihadharati, "usasa" mwaunenani?
Huwa ni Taifa duni, liso na Utamaduni.

Kamwe si vyote dhahabu, ving´aravyo minadani,
Nazo shaba zaghilibu, zinauzwa madukani,
Zishawatia aibu, walovaa harusini,
Huwa ni Taifa duni, liso na Utamaduni.

Mpingo mti mweusi, waota Afrikani,
Unauzwa kwa fulusi, ghali sana duniani,
Kudharau yetu sisi, tunatiwa ujingani,
Huwa ni Taifa duni, liso na Utamaduni.

Usemi wangu nifunge, wajumbe wetu Bungeni,
Sera hii muiunge, ili ipate mizani,
Nasi raia tuchange, mazuri yatuauni,
Lisiwe Taifa duni, liwe na Utamaduni.

Amiri A.S. Andanenga (Sauti ya Kiza)
Kinondoni - Shamba
Dar es Salaam
Tanzania. (*HAU)

KAJA NIZURU

Hoye! Hoye! Shangilizi, kutoka kwangu moyoni,
Hoye! Hoye! Za mbawazi, ziningile haibani,
Hoye! Hoywe! Maliwazi, sababu nawayuzani,
Kaja nizuru nyumbani, nduya´ Hassan Adamu.

Nduya Hassani Adamu, kaja nizuru nyumbani,
Ugeni wake muhimu, ulingiya dosarini,
Hatukumaliza hamu, kawa kiguu ndiyani,
Kulekea Jarumani, nduya´Hassani Adamu.

Alikitokeya Tanga, achenenda Jarumani,
Kwa mahaba kajifunga, kapija hodi langoni,
Kunizuru Andanenga, hapa Shamba Kinondoni,
Kwa yake kubwa hisani, nduya Hassani Adamu.

Ilikuwa asubuhi, hamuuza ndiwe nani?
Akiwa amefurahi, kanamba ndimi Hassani,
Akaniaga "nawahi", kwenye ndege kiwanjani,
Hatukulonga kwa ndani, nduya Hassani Adamu.

Kwa huo muda mchache, nawapani ya yakini,
Na kwa nini niwafiche, tabia yake mwendani,
Kanaifanya aniwache, asitoke kumbukoni,
Kwa njema yake lisani, nduya Hassani Adamu.

Hampa kisa halisi, chui kugeuka nyani,
Simba kugeuka fisi, chuma kugeuka kuni,
Jiti kugeuka nyasi, niwajuzao shikeni,
Kamakinika makini, nduya Hassani Adamu.

Tamati naihandisi, kwa matama na huzuni,
mwana wa nyoka mjusi, haogopwi abadani,
Hatunao wasiwasi, si mwenye sumu kanwani,
"JUA" lisihatiani, nduya Hassani Adamu.

Amiri A.S. Andanenga
(Sauti ya Kiza)
Kinondoni, Shamba
DAR ES SALAAM, Tanzania. (*HAU)

SIKU YA WANAWAKE DUNIANI WANAWAKE KATIKA UONGOZI KARNE YA 21

1. Karine zimepinduka, katika ukandamizi,
Wanawake kwa hakika, tumeonwa wapuuzi,
Hakuna bali kupika, na kuongeza kizazi,
Wanawake uongozi, kuongoza tunaweza.

2. Wanawake kuongoza, tunaweza uongozi,
Dunia kutupuuza, twayambia hatuwezi,
Hakuna cha kushangaza, sasa tunasema wazi,
Wanawake uongozi, kuongoza tunaweza.

3. Awezalo mwanadamu, kwa kutumia ujuzi,
Mwanamke ni lazimu, katika maandalizi,
Naye atalifahamu, bila ya kipingamizi,
Wanawake uongozi, kuongoza tunaweza.

4. Nayadhihirisha haya, katika ufafanuzi,
Waziri Golda Meya, Uyahudi kiongozi,
Nisemayo si hekaya, vita alivimaizi,
Wanawake uongozi, kuongoza tunaweza.

5. Hakuna cha ati ati, zamani na siku hizi,
Kuwini Elizabeti, nchi yenye ung´arizi,
Tangu kakalia kiti, uchumi wapanda ngazi,
Wanawake uongozi, tunaweza kuongoza.

6. India Indra Gandi, alifanya vyema kazi,
Spesioza mshindi, Rais muandamizi,
Hata katika ufundi, mabibi ni watambuzi,
Wanawake uongozi, kuongoza tunaweza.

7. Bibi Sadako Odaka, Shirika la Wakimbizi,
Rais wa Sirilanka, Kumaatunga mjuzi,
Uthibitisho hakika, hakuna la utatizi,
Wanawake uongozi, kuongoza tunaweza.

8. Bibi Tabita Siwale, wa Mataifa Balozi,
Mery  Nagu vilevile, ni Waziri wa Malezi,
Eda Sanga mteule, Radioni kiongozi,
Wanawake uongozi, kuongoza tunaweza.

9. Wanaume msipinge, kwa kazi za uguzi,
Aidha kwenye mabunge, sheria maandalizi,
Kwenye kukimbiza mwenge, udereva twamaizi,
Wanawake uongozi, kuongoza tunaweza.

10. Pia katika majeshi, ya vita kwa shambulizi,
Tunazimudu ambushi, aidha upelelezi,
Kazi za usuluhishi, ujaji na uenezi,
Wanawake uongozi, kuongoza tunaweza.

11. Karine hii ya haja, kusiwe na kizuizi,
Ya ishirini na moja, kusiweko na ajizi,
Uongozi wa pamoja, kusiwe na ubaguzi,
Karine ya uongozi, wanawake kuongoza.

Amiri A. S. Andanenga (Sauti ya Kiza)
DAR ES SALAAM, Tanzania. (*HAU)

 

 

*Shukurani nyingi kwa wanajopo na wajumbe waliokusanya na kutuletea mashairi ya Amiri Sudi Andanenga ”Sauti ya Kiza”: Hassan Adam(HAU) na Gertrude Malai(GT).



 

Copyright © 1999-2010 TANZANET Inc - The Tanzanian Electronic Networking Community. All rights reserved.
We welcome your questions & comments about this site.